Singida. Wafanyabiashara wa vitunguu katika Soko la Misuna, Singida wameiomba Serikali kuwasaka na kuwakamata wafanyabiashara kutoka Kenya na Uganda wanaonunua zao hilo moja kwa moja kutoka kwa wakulima kwa madai kuwa wanawanyonya wakulima na kuikosesha halmashauri mapato.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi,
wafanyabiashara hao walidai kuwa baadhi ya madiwani katika maeneo
yanayolimwa vitunguu huwasaidia wafanyabiashara hao kununua vitunguu
kutoka kwa wakulima badala ya kununua kwenye soko.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Joseph Nadoo
alisema mbaya zaidi, wafanyabiashara hao hutumia magunia aina ya neti
yenye ujazo mkubwa ukilinganisha na magunia ya kawaida.
“Hawa wafanyabuiashara kutoka Kenya na Uganda
wakati mwingine tunaambiwa wananunua vitunguu vikiwa shambani
(havijavunwa), huku ni kuwapunja wakulima, lazima Serikali ya Mkoa
iliangalie hili badala ya kulifumbia macho,” alisema mmoja wa
wafanyabiashara katika Soko la Misuna ambaye alikataa kutajwa jina kwa
usalama wake.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Faustine
Kiyui alisema ofisi yake haina taarifa kama wafanyabiashara hao huwa
wanakwenda moja kwa moja kwa wakulima na hutumia magunia yenye ujazo
mkubwa.
Alisema watachunguza na wakibaini, hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Serikali mkoani hapa kwa miaka mingi, imekuwa
ikipiga marufuku wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kununua
vitunguu moja kwa moja kutoka kwa wakulima na badala yake ikiwataka
wanunue katika soko maalumu la zao hilo la Mihuna, marufuku ambayo
imeshindikana.
No comments:
Post a Comment